Mwanzilishi wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba ‘Bongo star Search (BSS)’, Rita Paulsen maarufu kama Madam Rita amesema kuwa shindano hilo halijafa kama baadhi ya watu wanavyodhani bali litarejea kwa kishindo.

Madam Rita ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark Production ambao ni waandaaji wa shindano hilo linalosaka vipaji vya kuimba nchi nzima na kutoa zawadi ya mamilioni ya shilingi za Kitanzania kwa washindi amesema kuwa wanajipanga kulifanya shindano hilo kuwa bora zaidi.

“Tumeipa break (mapumziko). Unajua ili kufanya BSS lazima uwe na good sponsorship (udhamini mzuri). Kwahiyo tunatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha. Mwaka huu tukifanya itakuwa ni miaka 10 ya Bongo Star Search,” Madam Rita aliiambia Maisha Mseto ya 100.5 Times Fm.

“Haiwezi kufa kirahisi, hatujajua kama tutafanya mwaka huu au mwakani lakini tutatangaza,” aliongeza.

BSS ilipata umaarufu na kuibua vipaji kadhaa vya watu waliogeuka kuwa wasanii wakubwa nchini kama vile Kayumba Juma, Kala Jeremiah na wengine. Umaarufu wa shindano hilo pia ulitokana na majaji wake, Salama Jabir pamoja na wa tayarishaji wa muziki Master Jay (MJ Records) na P-Funk Majani (Bongo Records).

Mara ya mwisho, BSS ilifanyika mwaka 2015 ambapo Kayumba Juma aliibuka mshindi na kunyakua shilingi milioni hamsini.

Steve RnB aweka wazi ‘bifu’ kati yake na Man Walter
Video: Itazame ngoma mpya ya Rayvanny 'Unaibiwa'