Jeshi la Polisi mkoani Arusha katika operesheni maalumu ya ukaguzi wa leseni za kuendesha vyombo vya moto limewafutia madaraja madereva 109 kwa kukosa sifa baada ya kufanya ukaguzi kwa madereva 522.
Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Msaidizi wa Polisi, Justine Masejo amesema zoezi hilo ni la hiari hadi Aprili 30, 2023 likihusisha madereva wenye leseni zenye madaraja ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubeba abiria pamoja na mizigo.
Amesema madereva wote wenye leseni zisizokuwa na sifa hasa wanaondesha magari ya abiria na mizigo lakini pia kwa wale ambao tayari wamefutiwa madaraja yao kwenda kusoma udereva katika vyuo vya Serikali katika kipindi kilichobaki.
Aidha amebainisha kuwa baada ya kipindi hicho cha hiari kupita watafanya msako mkali kwa madereva wote waliokaidi ukaguzi huo na kwamba madereva wote pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na ajali.