Madereva 23 wa malori ya mizigo kutoka Tanzania wamezuiwa kuingia nchini Kenya kupitia mpaka wa Namanga leo, Mei 13, 2020 baada ya kubainika kuwa na maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19).

Katibu Mkuu wa Wazira ya Afya wa Kenya, Dkt. Rashid Aman ametoa taarifa hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapambano dhidi ya covid-19.

Amesema kuwa mbali na Watanzania hao, raia mmoja wa Uganda na mwingine wa Rwanda pia wamekataliwa kuingia nchini humo baada ya kubainika kuwa na virusi hivyo.

Jana, madereva wawili wa malori raia wa Tanzania walikataliwa kuingia nchini humo wakiwa kwenye mpaka wa Isbania baada ya kubainika kuwa na virusi vya corona.

Katika hatua nyingine, madereva wa Tanzania walio katika mpaka wa Namanga wanaotaka kuingia nchini Kenya wamelalamika kuwa utaratibu wa kuwapima virusi vya corona huchukua muda mrefu na huwagharimu zaidi.

Dereva mmoja kutoka Dar es Salaam aliyekuwa akisubiri kuingia nchini Kenya, Issa Hamisi aliliambia gazeti la The Citizen kuwa kulikuwa na zaidi ya madereva 400 waliokuwa wanasubiri majibu ya vipimo vya corona leo.

Aidha, walilalamikia utaratibu unaotumika kuwapima wakihofia afya zao kutokana na jinsi maafisa wa afya wanavyowapima.

“Utaratibu unaotumika kutupima nao unazua maswali mengi kwa sababu maafisa wanaopima watu hapa wengine hawanawi mikono baada ya kumpima mtu mmoja, kwahiyo tunapata wasiwasi kuwa tunaweza kupata maambukizi ya covid-19 wakati wa mchakato wa kupima,” Hamisi anakaririwa.

Alitoa wito kwa Serikali kufanya utaratibu wa kuzungumza na wenzao wa Kenya ili kupata njia bora zaidi na rafiki.

Leo, Kenya ilitangaza kuwa na visa vipya 22 vya corona, hatua inayofanya jumla ya visa vya corona kufikia 373. Vifo vinavyotokana na corona ni 40 na watu 281 wamepona, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya nchi hiyo.

Waumini 44 wa parokia moja wafariki kwa corona, mchungaji aeleza

Ibada ya mazishi yashambuliwa kwa mabomu, 24 wafariki

TP Mazembe mabingwa DR Congo
Waumini 44 wa parokia moja wafariki kwa corona, mchungaji aeleza

Comments

comments