Hatimaye madereva 12 wa malori ya Tanzania na Kenya waliokuwa wametekwa katika Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wameokolewa.

Waziri wa Mambo ya ndani wa DRC ameiambia BBC kuwa madereva wote wameokolewa na vikosi vya nchi hiyo na kwamba wote wako salama.

Aidha, alisema kuwa watu walioendesha utekaji huo ni kundi la majambazi ambalo bado hawajalifahamu ni lipi, lakini sio vikosi vya waasi wa Maimai kama ilivyoelezwa awali.

“Ni kusema ni majambazi tu walitoka porini, walipoona magari yanatembea wakayasimamisha na kuangalia kama kuna pesa, walipokuta hakuna pesa wakawachukua madereva wakakimbia nao porini,” amesema Waziri huyo wa Congo.

Madereva hao walitekwa Septemba 14 mwaka huu na waasi hao waliotoa saa 24 kwa masharti ya kupewa dola 4,000 kwa kila mateka ili waweze kuwaachia.

Aidha, Serikali ya Congo imeeleza kuwa ni magari saba pekee ya kampuni ya Simba ndiyo yaliyochomwa moto kati ya magari 12 yaliyovamiwa na majambazi hao.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopeleka wanajeshi wake katika kikosi cha Umoja wa Mataifa kwa lengo la kulinda amani nchini DRC ambako waasi wamekuwa wakiwaua na kuwaonea raia wa nchi hiyo.

Mbowe roho juu, hukumu yake kusomwa leo.
‘Ya Ommy Dimpoz na Ali Kiba ni Hatari nyingine’