Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa, katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2021-2022, kati ya mwezi Julai hadi Desemba, 2021 tume ilikusanya shilingi bilioni 311 zilizotokana na kodi mbalimbali kwenye uchimbaji na biashara ya madini.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo kwenye mahojiano maalum na vyombo vya habari katika kikao kazi cha Tume ya Madini kilichoshirikisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa mjini Morogoro chenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi ili kufikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021-2022 la shilingi bilioni 650 lililowekwa na Serikali.

Mhandisi Yahya Samamba akizungumza mbele ya waandishi wa habari.


Kikao hicho kimehusisha pia Makamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma na Janeth Reuben Lekashingo.


Amesema kuwa, siri ya tume kuendelea kufanya vizuri ni pamoja na uchapakazi na uzalendo wa watumishi wa Tume ya Madini nchini kote, usimamizi mzuri wa masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini kwa lengo la kukuza mapato na kudhibiti utoroshaji wa madini.


Akizungumzia mchango wa masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, Mhandisi Samamba amesema kuwa ni pamoja na wachimbaji wa madini kupata soko la madini yao na kuuza madini yao kulingana na bei elekezi inayotolewa na Tume ya Madini kulingana na Soko la Dunia.


Akielezea mikakati mingine ya kuongeza ukusanyaji wa maduhuli kwenye Sekta ya Madini ameeleza kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa mfumo maalum wa ukusanyaji wa maduhuli kwa njia ya kielektroniki kwenye madini ujenzi ambao utasaidia wachimbaji wa mchanga na wazalishaji wa madini ujenzi kulipa kodi mbalimbali kwa urahisi na serikali kukusanya mapato stahiki.


Ameongeza kuwa mfumo husika utawezesha Serikali mbali na kupata mapato zaidi utasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za madini ujenzi na viwandani.


Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma amesema kuwa kukutana kwa viongozi wa Tume ya Madini wakiwemo Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kutasaidia kubaini changamoto wanazokabiliana nazo kwenye utendaji kazi na kuzipatia ufumbuzi.
Katika hatua nyingine amewataka Viongozi wa Tume kuendelea kuchapa kazi kwa bidii kwa ubunifu na uadilifu mkubwa ili kuendelea kujenga taswira chanya ya Sekta ya Madini.

Vita ya wenyewe Ethiopia, Maafa yahamia kwa watoto
Wizara ya Ardhi yaja na suluhu kero za ardhi