Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, amesema mchango wa Sekta ya Madini katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni umekuwa ukiimarika ambapo kwa mwaka 2022 Sekta ya Madini imechangia asilimia 56 ya mauzo yote ya bidhaa zilizouzwa nje ya nchi.

Mbibo ameyasema hayo mara baada ya kutembelea wadau mbalimbali wa madini katika banda la Wizara ya Madini katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema, wadau wanatakiwa kuzitumia taasisi zilizo chini ya wizara Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ili Sekta ya Madini iweze kuchangia zaidi katika Pato la Taifa.

Katika hatua nyingine, Mbibo amezungumza na wadau wa Sekta ya Madini waliopo katika banda hilo ambao wamemweleza huduma wadau wanazotoa, fursa zilizopo katika maeneo ya shughuli zao.

Naibu Katibu Mkuu Mbibo aliongozana na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba na wadau wengine wa Sekta ya Madini.

Kagera Sugar yaanza kusajili kimya kimya
Rais Chakwera ampokea Balozi Kayola