Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, jana waliingia katika mvutano mkubwa na madiwani wa CCM na kujikuta wakishikana mashati.

Tukio hilo lilitokana na mvutano wa kiutaratibu katika uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa manispaa hiyo ambapo viongozi wa Ukawa walipinga uwepo wa wabunge wa viti maalum wa CCM waliotoka Zanzibar kushiriki zoezi la uchaguzi huo.

Wakiongea na waandishi wa habari, mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee walieleza kuwa wenzao wa CCM wanataka kuvunja sheria kwa kuwaleta wabunge hao wa viti maalum kutoka Zanzibar.

“Lengo lao ni kuhakisha kwamba wanashinda Halmashauri na hatimaye jiji. Lakini sisi tunafahamu kwamba nchi yetu inaendeshwa na sheria. Ukiangalia katiba ya Muungano kwa mfano, katika yale masuala 21 ya muungano, masuala ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sio ya Muungano,” alisema Halima Mdee.

Tafrani kati ya madiwani hao na wabunge ilipelekea wanachama wao waliokuwa nje ya ukumbi huo kutawanywa na jeshi la polisi huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty alilazimika kuahirisha zoezi hilo.

Natty alisema kuwa alilazimika kuahirisha zoezi hilo la uchaguzi ili aweze kupata ufafanuzi kutoka TAMISEMI kuhusu uhalali wa wabunge kutoka Zanzibar kupiga kura katika halmashauri hiyo.

Kambi Za Kijeshi Burundi Zashambuliwa
Ray C: Nimefilisika, Nimekimbiwa