Halmashauri ya Mji wa Makambako Mkoani Njombe imeeleza kuwa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Kondomu za kujikinga na maambukizi ya Ukimwi, jambo ambalo limewafanya baadhi ya madiwani kuitaka Wizara ya Afya kutatua changamoto hiyo.

Hoja hiyo imeibuliwa na Diwani wa viti maalumu halmashauri ya mji wa Makambako, Stella Uhemba wakati akihoji kuwa ni lini Serikali ya mji wa Makambako itamaliza tatizo la uhaba wa Kondomu hizo ambazo ni kinga ya magonjwa mbalimbali kwa binadamu ikiwemo ugonjwa wa Ukimwi.

Aidha, akijibu hoja hiyi iliyoibuliwa na diwani huyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makambako, Hanana Mfikwa amekiri kuwepo kwa tatizo hilo hali iliyo mlazimu kumwagiza Mganga Mkuu wa Hospitali ya Makambako kuwasiliana na mamlaka husika ili kutatua changamoto hiyo ndani ya wiki moja kuanzia sasa.

‘’Yaani ukipita katika nyumba mbalimbali za kulala wageni hapa mjini makambako nakuhakikishia utaona uhitaji wa Salama (Kondomu) kwa watu wetu ni mkubwa kuliko hata vyumba vya kulala hata mimi mwenyewe ninamiliki Nyumba ya kulala wageni hapa mjini nalitambua hilo, Mganga nakuagiza lishughulikie hilo,”amesema Mfikwa

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Makambako Dkt. Ernest Kyungu amekiri Uwepo wa tatizo hilo la uhaba wa Kondomu katika Halmashauri hiyo ya mji wa Makambako na kuahidi kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

Wadau wa Soka wamlilia Sala baada ya mwili wake kupatikana
Mkuchika awaangukia Ma RC, DC, 'Msiniponze jamani'