Maelekezo ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ya kutaka mchakato wa mwaka huu wa utoaji wa Tuzo za Muziki bila upendeleo yamefika mahali pazuri.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Matiko Mniko, imeeleza kuwa jumla ya kazi 402 zimewasilishwa kuanzia Februari 9, 2022 baada ya zoezi la kuwaelimisha wadau kukamilika na kuwa BASATA limeamua kuongeza muda wa siku saba, ili kutoa nafasi kwa wasanii wengi kushiriki.
Akizungumza kwenye Hafla ya Uzinduzi wa Utoaji wa Tuzo za Muziki na Ugawaji wa Mirahaba kwa Wasanii, Januari 28, 2022, kwenye Ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa aliielekeza BASATA kutenda haki ili kupata kazi zenye viwango bora.
“Tunaongeza siku 7 kwa ajili ya wasanii kuwasilisha kazi katika vipengele vya Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2021),” imefafanua taarifa hiyo na kuongeza kuwa mwisho wa kuwasilisha kazi hizo ni Machi Mosi mwaka huu.kupitia link www. tanzaniamusicawards.info