Maelfu ya wananchi, wengi wakiwa ni vijana wameandamana katikati ya mitaa ya jiji la London leo wakitaka kubatilishwa kwa matokeo ya upigaji kura yaliyosababisha Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (EU).

Maandamano hayo makubwa yamefanyika ikiwa ni wiki moja baada ya nchi hiyo kuanza kuathirika kwa kiasi kikubwa hususan kiuchumi kutokana na matokeo ya kuwa nje ya Umoja wa Ulaya.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango mengi walidai kuwa nchi hiyo haiwezi kupiga hatua ikiwa nje ya umoja huo, hivyo walitaka uamuzi huo wa wengi ubatilishwe.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, baadhi ya waandamanaji wametaka kuitishwa kwa upigaji kura huo kwa mara nyingine baada ya wananchi kuona madhara yaliyotokea kwa kipindi hiki kifupi wakiamini watabadili uamuzi wao kwenye sanduku la kura.

Asilimia 60 ya wapiga kura jijini London waliamua kubaki EU, lakini wananchi wa maeneo mengine waliwezesha kupata kura nyingi zaidi za jumla zilizotaka kujitoa.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliyekuwa anasisitiza nchi hiyo isijiondoe kwenye umoja huo, alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa na anatarajia kukabidhi rasmi ofisi mwezi Oktoba mwaka huu.

Madhara yaliyoanza kuonekana hivi sasa kwa kasi ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya kibaguzi, vitisho vya kigaidi na kuporomoka kwa pound ya nchi hiyo.

Facebook 'wampiga tofali' mwanamke anayeitwa ‘Isis’, alalama
Kiongozi mpya wa Taliban atoa sharti la kwanza kwa Marekani