Maelfu ya watu wameandamana nchini Ufaransa kumuunga mkono Samuel Paty, mwalimu aliyekatwa kichwa kwa kuonesha wanafunzi vibonzo vya Mtume Muhammad.
Watu katika eneo la de la République mjini Paris walikuwa wameshika vipeperushi vilivyoandikwa “Je suis enseignant” (Mimi ni mwalimu) huku waziri mkuu akijumuika na waandamanaji na kubeba kipeperushi kilichoandikwa “Sisi ni Ufaransa!”
Watu 11 wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi ingawa bado hakuna taarifa zilizotolewa kuhusu kukamatwa kwao na wakati huohuo mwanaume mmoja anayeitwa Abdoulakh A alipigwa risasi na polisi siku ya Ijumaa baada ya kumuua Mwalimu Paty karibu na maeneo ya shule karibu na mji wa Paris.
Rais Emmanuel Macron amesema ukatwaji kichwa cha mwalimu huyo katika kitongoji kilichopo kaskazini magharibi mwa mji wa Paris ni “Shambulio la kigaidi” na mwalimu huyo aliuawa kwa sababu alikuwa anafundisha uhuru wa kujieleza.
Mauaji hayo yanakuja baada ya shambulio la mwaka 2015 la Charlie Hebdo ambalo lililengwa na washambuliaji kwa kuchapisha katuni za Mtume Mohammad.