Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Freeman Mbowe amepokelewa na maelfu ya watu mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa Kilimanjari(KIA) mapema leo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mbowe kwenda Hai tangu atoke gerezani Machi 4, mwaka huu ambako alikaa kwa miezi minane akikabiliwa na tuhuma za ugaidi na uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ya Mbowe na wenzake watatu iliyokuwa ikiendeshwa katika Mahakama ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi ilifutwa baada ya Mandesha Mashtaka Nchini (DPP), kupeleka hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka hayo.
Tangu alipotoka Mbowe, amekuwa akifanya mikutano mbalimbali ikiwemo kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alimuita Ikulu jijini Dar es Salaam na kukubaliana kufanya siasa za kistaarabu na kujenga Taifa
Wananchi kwa wingi wakiwa na usafiri wa bodaboda, bajaji, magari na wengine wakitembea kwa miguu, walijikusanya katika njiapanda ya Kia Moshi huku Jeshi ka Polisi likiimarisha ulinzi na kuongoza msafara huo.
Alipofika katika Eneo hilo, Freeman Mbowe ambaye alikiwa kwenye gari la wazi akiwapungia wananchi na kuwashukuru kwa kusema “asanteni kunipokea tupo pamoja”.
Mapokezi hayo yalisababisha baadhi ya barabara kufungwa kwa muda kutokana na wingi wa watu, magari na pikipiki .