Jumla ya Vijiji 3,917 nchini vinatarajiwa kufikiwa na huduma ya umeme katika awamu ya tatu mzunguko wa pili na kufanya jumla ya vijiji vyote 12,345 vya Tanzania Bara kuwa na nishati hiyo.
Hayo yamebainishwa Bungeni Jijini Dodoma hii leo Juni Mosi, 2022 na Waziri wa Nishati January Makamba wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Kuna malalamiko kuwa umeme wa vijijini unazifikia kaya chache hivyo Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupata fedha zaidi kwa ajili ya kuongeza kilometa mbili kwa kila kijiji tofauti na kilometa moja ya sasa,” amesema Makamba.
Amesema tayari wakandarasi wameagizwa kufanya tathmini ya kupeleka umeme kwenye vijiji vilivyokosa awamu ya kwanza ya mradi na kwamba Serikali italiwezesha Shirika kuendelea na mageuzi ya kutoa huduma bora.
Aidha katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema Shirika linatarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa kubadilisha mita za Luku zinazotumika sasa kwa kuweka mita janja.
“Hatua hii itawezesha wateja kununua umeme na utaingia moja kwa moja kwenye mita zao na kuwaondolea usumbufu wa awali wa token na hii pia italisaidia shirika kuongeza mapato,” ameongeza Waziri huyo wa Nishati.
Waziri Makamba ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 164.54 zitakazotumika na Wizara ya Nishati katika mwaka wa fedha 2022/2023.