Scola Msewa – Pwani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena amesema Wilaya ya Mafia ni kitivo cha mazalia ya samaki Duniani kutokana na uwepo wa matumbawe hai yaliyopo eneo hilo na Samaki wengi kuzaliana humo.
Meena amesema hayo wakati akifunga Kongamano la Wadau wa uwekezaji katika uchumi wa Buluu Willayani Mafia, lililo ambatana na maonesho ya siku tatu ya shughuli mbalimbali za Wadau wa uwekezaji wa Utalii nchini.
Amesema, kama ilivyo kwa upande wa Wanyama Serengeti ndio kitivo cha vivutio mbalimbali vya Utalii wa Wanyama Duniani na kwa upande wa Samaki, Wilaya ya Mafia ndio kitivo cha mazalia ya samaki Kidunia.
Aidha ameongeza kuwa, Wilaya ya Mafia pekee ni kivuko cha uwekezaji katika uchumi wa Buluu ikiwemo Uvuvi endelevu na Serikali tayari imeanza mchakato wa kuwezesha Wananchi kiuchumi, ili waweze kufanya shughuli halali za Uvuvi ikiwemo kilimo cha mwani na mazalia ya Samaki katika vizimba, ili kuinua shughuli za Uvuvi na ufugaji wa viumbe.
Awali akizungumzia mkakati wa Serikali kuhakikisha Wilaya ya Mafia inafikika kiurahisi na Wananchi na Watalii, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Zephania Sumaye amesema tayari wametenga fedha kwaajili ya kuleta kivuko kikubwa kipya na uboreshaji wa uwanja wa ndege.