Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam na maeneo mbali mbali ya nchi kwa takribani wiki sasa, zimesababisha mafuriko makubwa katika Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani ambapo maji yamejaa na kuifunga kabisa barabara hiyo.
Dar24 Media tumefika eneo la Jangwani na kujionea hali ilivyo ili tuweze kukuletea habari kamili kutoka katika maeneo hayo yalioathiriwa na mvua kwa kiasi kikubwa, ambapo tumezungumza na wananchi ambao wameeleza kuwa barabara hiyo imefungwa hakuna usafiri na wao hawawezi kuvuka kwani maji ni mengi kuliko kawaida, hali inayopelekea kushindwa kufika katika shughuli zao za kila siku.
Wananchi hao wamesema kutokana na adha hiyo wanapata msaada wa kuvuka kutoka kwa waendesha maguta kwa shilingi elfu moja kwa kila mwananchi.
Aidha, hakuna kifo, majeruhi wala maafa makubwa yaliyoripotiwa kutokana na mafuriko hayo mpaka sasa.