Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Leo (Januari 13, 2023), imezua taharuki kwa wakazi wa kata za Lukobe, Kihonda na Mkundi zilizopo katika Manispaa ya Morogoro, ambapo mafuriko yameyakumba maeneo hayo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, Wakazi wa maeneo hayo wamesema mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya saa nane usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi na kuleta madhara ya nyumba kuanguka, huku vitu mbalimbali vikisombwa na maji.
Mkuu wa wilaya Morogoro, Albert Msando amefika katika maeneo hayo na kuagiza shule zilizopo katika maeneo hatarishi yenye mafuriko kufungwa kwa muda licha ya kuwa hakuna madhara yoyote kwa binadamu yaliyoripotiwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini, Ablulazizi Abood amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa na utulivu wakati serikali ikifanya tathimni ya madhara yaliyojitokeza.