Mamlaka za usalama nchini Rwanda, zimesema takriban watu 109 wamefariki dunia magharibi mwa nchi hiyo baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko katika eneo hilo mapema hii leo Jumatano asubuhi Mei 3, 2023.
Shirika la Utangazaji la Rwanda liliandika kupitia akaunti yake rasmi, na kutoa picha za video ikisema, “idadi ya waliofariki kutokana na mvua kubwa na kusababisha mafuriko inaendelea kuongezeka, ambapo watu 109 sasa wamethibitishwa kufariki katika Mikoa ya Magharibi na Kaskazini.”
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, “Mvua kubwa ilinyesha usiku kucha, na kusababisha mateso makubwa katika wilaya za Ngororero, Rubavu, Nyabihu, Rutsiro, na Karongi,” huku Gavana wa Mkoa wa Magharibi, Francois Habitegeko akisema “mvua ilisababisha maporomoko ya ardhi na kufunga barabara.”
Habitegeko ameongeza kuwa, watu wengine ambao idadi yao bado haijajulikana rasmi walijeruhiwa na mafuriko hayo wengine kunaswa chini ya nyumba zao na kwamba kipaumbele kikuu cha wahudumu wa dharura ni kuwaokoa watu hao.