Wamiliki wa maghala ya mafuta nchini, wamesema wana Petroli na dizeli za kutosha na wapo tayari kutoa ushirikiano wa kuyasambaza kwenye maeneo mbalimbali yenye uhitaji Nchini, huku Wadau wakiiambia Serikali kuwa wanafanya kazi saa 24 hadi siku za mapumziko, ili kuhakikisha magari yanaingia na kutoka katika maghala.

Wadau hao, wamesema hayo Julai 23, 2023 mbele ya Waziri wa Nishati, January Makamba aliyeambatana Kamishna wa Mafuta na Gesi Asilia, Michael Mjinja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, Dkt. James Andilile ambapo Viongozi hao wamefanya ziara ya kukagua maghala hayo.

Meneja Mkuu wa Meru Petroleum, Charles Maingu amesema ndani ya siku 10 zilizopita wametoa mzigo wa mafuta wa lita milioni 28 yaliyosafirishwa ndani ya nchi na nje ya nchi, akisema Agosti pia watapokea mzigo mwingine dizeli milioni 27 na petroli lita milioni 40.

Amesema, “pia mzigo wa Septemba mafuta ya petroli ni lita milioni 19.5 na dizeli lita milioni 18. Waziri (Makamba), hapa shughuli zinaendelea huu mzigo unaotoka unakwenda nje ya nchi ndani ya Nchi tumeshawapelekea hasa maeneo ya pembezoni.


“Kama Kuna maeneo yoyote yenye changamoto ya upatikanaji wa nishati hii, tupewe taarifa tutaifikisha, nisema tu hakuna changamoto ya mafuta yapo ya kutosha,” amesema Maingu.

Mkurugenzi Mtendaji Puma Energy, Fatma Abdallah amesema Julai mwaka huu kumekuwa na mahitaji makubwa ya mafuta akisema hadi jana wameuza petroli na dizeli lita zaidi ya milioni 36. Amesema  hali hiyo ni tofauti na mwaka 2022 waliuza milioni 30.

Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Meli wa Wakala wa Uagizaji Mafuta Pamoja – PBPA, Bruno Tarimo amesema meli zote zilizopangwa kuleta mzigo wa mafuta kwa mwezi Julai zimefika kwa wakati na kusema hivi sasa meli ya pili inamalizia kupakua mzigo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati January Makamba amesema lengo ziara hiyo ni kujua hali ya mafuta yaliyopo katika maghala ya wafanyabiashara hao, sambamba kusikia na kuzibeba changamoto zinazowakabili wadau hao wa sekta hiyo.

Naye, Dk Andilile amesema wamepita takribani maghala sita yanayohifadhi mafuta, akisema wamehakikishiwa kuwa nishati hiyo ipo na Watanzania wasiwe na hofu. Akisema kwa sasa wanaendelea na utaratibu wa kuyasafirisha kupelekwa katika maeneo mbalimbali hasa pembezoni.

“Nchi ina mafuta ya kutosha, kinachofanyika hivi sasa ni kuyapeleka maeneo mbalimbali hasa pembezoni ambayo yalikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mafuta.Wamiliki wa maghala wametuhakikishia kuwa yatafika kwa wakati wananchi wasiwe na hofu,” amesema Dk Andilile.

Harry Kane amvuruga Kocha Ange Postecoglou
Hafiz Konkoni kukabidhiwa mikoba ya Mayele