Baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, kutangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini ambayo zimepungua na kuanza kutumika kuanzia Jumatano, Julai 5, 2023, Wananchi wametoa maoni yao huku wakisema itasaidia kuleta ahueni ya gharama za maisha.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Mwainyekule ilieleza kuwa bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeshuka kwa shilingi 137/Lita na shilingi 118/lita, mtawalia, ikilinganishwa na bei za toleo la tarehe 7 Juni 2023 ambapo Wananchi wanadai Serikali sasa ingalie namna ya kushusha bei za usafiri na huduma muhimu.
Katika taarifa hiyo ya EWURA, Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei ya rejareja ya mafuta ya petroli imeshuka kwa Shilingi 188/Lita wakati bei ya mafuta ya dizeli imeongezeka kwa shilingi 58/lita ikilinganishwa na bei za toleo la Juni 7, 2023.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya Wananchi hao akiwemo Daniel Mgube, Scolastika Mahenge, Hamis Bakari na Musa Kitalika wamesema wana imani na Serikali na kwamba ni mataraji yao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atatoa maelekezonkwa mamlaka husika kuona ni jinsi gani kushuka kwa bei ya mafuta kutaendana na punguzo la nauli na bidhaa muhimu.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya EWURA imelekeza kuwa, Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, huku ikionya kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja.
Bei katika mikoa na miji husika ni kama inavyoonekana katika majedwali hapa chini.