Wafungwa watatu ambao walihukumiwa kwa Ugaidi na kufanikiwa kutoroka kwenye Gereza lenye ulinzi mkali la Kamiti nchini Kenya juzi Jumatatu wamekamatwa leo asubuhi katika Msitu wa Enzio katika Kaunti ya Kitui, baada ya Raia kutoa taarifa kwa Polisi na inaaminika Wafungwa hao walikuwa wanatorokea Somalia.
Itakumbukwa Serikali ya Kenya ilitangaza kuwa atakayefanikisha kupatikana kwa Wafungwa watatu wa Ugaidi waliotoroka Gerezani nchini humo atapatiwa Milioni 60 za Kenya ambazo ni sawasawa na zaidi ya Bilioni 1.2 za Kitanzania.
Rais Kenyatta jana alifanya maamuzi ya kumfuta kazi Kamishna Mkuu wa Magereza nchini Kenya Wycliffe Ogalo siku chache baada ya Wafungwa hao kutoroka ambapo nafasi yake imechukuliwa na Brigedia Mstaafu John Kibao Warioba, Kamishna huyo na Mkuu wa Gereza la Kamiti wote wamekamatwa.
Waliotoroka ni Mohamedi Ali Abikar, ambaye alihukumiwa kwa kuhusika na shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa mwaka 2015 lililoua Watu 148 waliuawa, mwingine ni Mushraf Abdalla ambaye alihukumiwa mwaka 2012 kutokana na shambulio lililodhibitiwa dhidi ya Bunge la Kenya na watatu ni Joseph Odhiambo ambaye alihukumiwa mwaka 2019 kwa kujaribu kujiunga na kundi la wanamgambo wa Al- Shabab nchini Somalia.