Takribani watu 49 wameuawa na wengine makumi wamejeruhiwa vibaya baada ya watu wenye silaha wanaotajwa kuwa magaidi kuwashambulia kwa risasi waumini waliokuwa wakifanya ibada kwenye misikiti miwili tofauti jijini Christchurch nchini New Zealand, mapema leo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Jacinda Ardern tukio hilo lilikuwa limeratibiwa vizuri kigaidi na washambuliaji walitekeleza katika misikiti miwili tofauti, wakiua watu 30 kwenye msikiti mmoja wakati wa ibada ya Ijumaa.
Tukio hilo limewashtua wengi pamoja na nchi za jirani kwani nchi hiyo ina historia nzuri ya kuwa nchi ya amani.
Waziri Mkuu Ardern mekaririwa na CNN akieleza kuwa washambuliaji hao walikuwa na mtazamo wa imani kali ya kidini ambazo sio msingi wa utamaduni wa New Zealand pamoja na dunia kwa ujumla.
Polisi wamefunga barabara na misikiti yote miwili kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina wa eneo la tukio wakati majeruhi wakikimbizwa hospitalini.
Jumla ya watu 48, ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake wenye majeraha ya risasi walikimbizwa katika hospitali ya Christchurch kwa ajili ya matibabu.
Mkuu wa polisi wa nchi hiyo, Mike Bush amesema kuwa watu wanne wanashikiliwa kutokana na tukio hilo, ambao ni wanaume watatu na mwanamke mmoja.
Polisi wameeleza kuwa hawaamini kama kuna watuhumiwa wengine zaidi lakini uchunguzi unaendelea. Watu wote walioshikiliwa kwa mujibu wa Bush hawakuwa kwenye orodha ya watu walio chini ya uangalizi wa vyombo vya usalama.