Serikali imetangaza rasmi kuyafungulia magazeti manene ya Mwanahalisi, Mawio, Tanzania Daima na Mseto miezi kadhaa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aagize vyombo vya habari vilivyofungwa kufunguliwa.
Uamuzi huo umetangazwa leo Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni za magazeti hayo.
“Agizo la Rais ni sheria, natoa leseni kwa Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima, kwa sababu mambo haya ni vizuri tutoke kwenye maneno twende kwenye matendo, tufungue ukurasa mpya, ili tumalize maneno, mwenye maneno yake aanze yeye, ukikutana na jiwe unarudi nyuma, unalipisha, kikubwa kazi iendelee,” Waziri wa Habari, Nape Nnauye
Akizungumza mara baada ya kupokea leseni za magazeti yake ambayo ni Mwanahalisi na Mseto, Said Kubenea ambaye ni mmiliki wa magazeti hayo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu kwa kufungua ukurasa mpya na vyombo hivyo vya habari huku akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali.