Mchakato wa kura za maoni kuwania nafasi za kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilikamilika jana katika sehemu nyingi nchini huku tuhuma za hujuma zikitawala.

Taarifa za matokeo ya kura hizo za maoni ziligubikwa na lawama nyingi kutoka kwa baadhi ya wagombea walioshiriki katika mchakato pamoja na watu waliokuwa wakiwaunga mkono.

Baadhi ya majimbo yaliyolalamikiwa kwa kile kinachofahamika zaidi hivi sasa kama ‘goli la mkono’ ni pamoja na jimbo la Iramba Magharibi ambapo naibu waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba alitangazwa kuwa mshindi kwa asilimia zaidi ya 90. Mwigulu alikuwa katika mtafaruku na baadhi ya wagombea wenzake ambao siku chache kabla ya zoezi la upigaji kura walimtuhumu kwa kutoa rushwa na kuwashawishi wasimamizi kumpendelea. Hata hivyo, baada ya kuhojiwa na Takukuru hakukutwa na hatia. Wagombea walioshindwa katika jimbo hilo wamewasilisha malalamiko yao katika makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma.

Tuhuma zilizojitokeza katika jimbo la Nchemba zilifanana na zile zilizojitokeza pia katika jimbo la Mtama ambapo Katibu Itikidi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alishikiliwa na Takukuru Mkoa wa Singinda, waliomtilia shaka baada ya kupata taarifa kuwa alitoa kiasi fedha benki kwa lengo la kuwahonga wajumbe. Hata hivyo, Takukuru walithibitisha baada ya kumhoji kwa muda kuwa kiasi cha fedha alichokitoa benki (Milioni 3,600,000) hakikuwa kwa ajili ya kutoa rushwa kwa wajumbe kama ilivyodaiwa awali. Nape alifanikiwa kushinda katika jimbo hilo kwa kishindo.

Katika jimbo la Kongwa, naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai ambaye jana alitangazwa kuwa mshindi kwa ushindi wa kishindo, alilalamikiwa na wagombea wenzake kwa tuhuma za kutumia fedha na wadhfa wake kufanya hujuma. Ndugai ana tuhumiwa kwa kumpiga fimbo mgombea mwenzake siku chache zilizopita na kumsabisha kupoteza fahamu na kulazwa hospitali. Hata hivyo, Ndugai alikanusha na kudai kuwa alipiga simu iliyokuwa ikichukua video na sio mtu aliyekuwa akichukua video hiyo.

Jijini Dar es Salaam katika jimbo la Segerea, naibu waziri ajira na kazi, Makongoro Mahanga alitangaza kukihama chama hicho baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro hicho akidai kutotendewa haki.

Hali ilikuwa tete pia katika jimbo la Tarime Mjini ambapo tuhuma za hujuma zilipelekea kuahirisha kutangaza matokeo usiku hadi siku ya leo. Wagombea katika mchakato huo, Gaudencia Kabaka na Nyambare Nyang’wine walituhumiwa kuhujumu mchakato baada ya karatasi za kura kupatikana kwenye masanduku zikiwa na alama ya vyema kwenye majina yao hata kabla ya upigaji kura. Mchakato umeahirishwa kwa muad hadi hapo baadae.

Matokeo ya kura za maoni za CCM katika majimbo mengi zimepelekea kuwepo mtafaruku katika majimbo mengi ambapo majeruhi wa matokeo hayo hasa wale wanaodhani kuwa wamehujumiwa kwa ‘goli la mkono’ wanaweza kukihama chama hicho wakikimbilia upinzani.

 

Ole Sendeka Azungumzia Taarifa Za Kuhamia Chadema
Makongoro Mahanga: CCM Walinionya Kuhusu Lowassa