Mshauri wa Bodi ya Wakurungenzi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Crescentius Magori, amesema walikua na wakati mzuri sana walipokua nchini Botswana kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Hatua ya Kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy uliochezwa Jumapili (Oktoba 17) mjini Gaborone.
Katika mchezo huo Simba SC ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Mshambuliaji na Nahodha wa kikosi chao John Raphael Bocco dakika ya 02 na 05.
Magori amesema wenyeji wao (Jwaneng Galaxy) walikua waungwana, na hawakuwa na dalili zozote za kuwafanyia Figisu kama ilivyozoeleka katika baadhi ya klabu na nchi walizowahi kwenda kucheza michuano ya kimataifa.
Hata hivyo amesema Simba SC ni klabu yenye uungwana siku zote, haiwezi na haitaweza kufanya vitendo vya hujuma, hivyo wanawakaribisha Jwaneng Galaxy kwa mikono miwili jijini Dar es salaam.
Amesema Jwaneng Galaxy wakiwa jijini humo watapata watakaowapokea na watakaowashangilia wakati wa mchezo huku akitumika jina la ‘Uto’ akimaanisha watani zao wa jadi Young Africans.
“Sisi Wanamsimbazi ni waungwana hivyo wasitarajie kuwa watafanyiwa jambo lolote lisilo la kiungwana”
“Tena huku kwetu kuna ‘Uto’ ambao ndio Kamati ya mapokezi, wanaweza hata kwenda uwanja wa Ndege kuwapokea…!” amesema Magori
Magori ambaye alikuwa sehemu ya msafara wa Simba SC uliokuwa Botswana, ameongeza kuwa baada ya kurejea nchini timu imeingia kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano ambao utapigwa Jumapili (Oktoba 24) katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es salaam.
Jwaneng Galaxy wanatarajiwa kuwasili nchini leo Jumatano (Oktoba 20) kuelekea mchezo huo ambao Simba tayari iko mbele kwa mabao 2-0.