Kiungo mkabaji kutoka nchini Brazil Gerson Fraga ametajwa kuwa kikwazo cha kuipa ushindi Simba SC kwenye mchezo dhidi ya Young Africans uliochezwa Jumamosi Novemba 07, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.
Fraga hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kwenye mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, kutokana na kuwa majeruhi, huku tayari akiwa ameshakosa baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Jina la kiungo huyo ambaye alifunga bao la kwanza dhidi ya Young Africans kwenye mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao manne kwa moja miezi mitatu iliyopita, limeibuliwa na mshauri binafsi wa Mwekezaji wa Simba, Mohamed “Mo” Dewji, Crescentius Magori.
Amesema kwa uchezaji ambao Young Africans walikuwa wanacheza kwa kutumia zaidi nguvu sehemu ya katikati ya uwanja, Fraga angeweza kabisa kusaidiana vema na Jonas Mkude kuwadhibiti.
“Pengo la Fraga ambaye anafanya shughuli pale katikati lilionekana. Kwa sababu sidhani kama wachezaji wa Young Africans wangepita pale. Ilikuwa ni shida sana kukosekana kwake kwa sababu yeye amekuwa akiwasaidia na kuwalinda mabeki wa kati na pia uchezaji wa kutumia nguvu ungeenda sawa na wale wenzetu, hivyo kungekuwa na shughuli,” amesema Magori.
Fraga, aliumia dakika za mwanzo kwenye mchezo kati Simba SC dhidi ya Biashara United Mara Septemba 20, na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla.