Kusuasua kwa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Burigi Wilayani Chato kumemsababisha Rais John Magufuli kuibana Wizara ya Afya ili kuhakikisha ujenzi wa Hospitali hiyo rufaa inakamilika katika muda uliopangwa ili wananchi wapate huduma za kiafya.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Januari 11, 2021 baada ya Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi kuweka jiwe la msingi katika hospitali hiyo ambapo pia amemuhakikishia mgeni wake kuwa atasimamia kukamilika mapema kwa hospitali hiyo.
Pia Rais Magufuli amezungumzia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji, amesema biashara kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka hadi Sh. bilioni 93.6 mwaka 2020
Ameongeza kuwa urafiki kati ya Tanzania na Msumbiji ni wa muda mrefu tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kwamba ndani ya Serikali wameweka makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja.
Naye Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, amesema kuwa leo mara baada ya kufika katika anga la Chato, aliona mashimo mengi chini ikiwa ni kiashirio cha uchimbaji wa dhahabu na kusema kuwa Geita ni Mkoa tajiri.
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi, yupo nchini kwa ziara ya siku mbili kuanzia leo Januari 11 na 12 2021.