Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ameendelea kupaza sauti yake akiahidi kupambana vilivyo na wala rushwa na wezi wa mali ya umma.

Dk. Magufuli amepaza sauti yake jana wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mikoa ya Katavi na Rukwa ambapo aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha elimu ya msingi na sekondari hadi kidato cha nne inatolewa bure kwa kuwa fedha zipo ila kuna watu wachache wanaojinufaisha.

“Fedha zipo lakini kuna wala rushwa wachache ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali, nawaomba mnichagueni nitapambana nao,” alisema Dk.Magufuli.

Ingawa alionesha kukubali kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya awamu ya nne, Dk. Magufuli alionesha kuzitambua changamoto zilizobaki na kuahidi kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vitakavyoinua sekta ya kilimo nchini.

“Ninashangazwa leo inafanyika wiki ya maziwa wakati maziwa hakuna, inafanyika wiki ya maji wakati kuna shida ya maji, wiki ya ukimwi na dawa hakuna, nitarekebisha hili kwa vitendo,” alisisitiza na kuongeza kuwa anafahamu kero ya ukosefu wa dawa katika hospitali. Alisema anafahamu wananchi wanaelekezwa kununua madawa kwenye maduka binafsi ya dawa pale wanataka huduma hiyo katika hospitali ya Umma.

Umati ukimsikiliza Dk. Magufli

Umati ukimsikiliza Dk. Magufuli

Alisema akipewa ridhaa atahakikisha analiondoa tatizo hilo na dawa zinapatikana katika hospitali za serikali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alijitokeza kwa mara ya kwanza jukwaani kumuunga mkono Magufuli katika jimbo la Katavi ambapo alitumia fursa hiyo kukanusha minong’ono iliyokuwepo kuwa huenda hakubaliani na uteuzi wa mgombea huyo kwa kuwa yeye pia jina lake lilikatwa.

“Kuna mtu alinipigia simu akaniuliza ‘mbona haukuonekana kwenye uzinduzi?’ nikamuuliza ‘Kwayo..!!’ Napenda kuwahakikishia wote kuwa mimi ninamuunga mkono huyu jamaa kwa asilimia 100,” alisema Pinda.

Pinda alieleza kuwa Magufuli anafaa zaidi kuwa rais wa Tanzania kutokana na histori yake ya utendaji kazi hivyo akawataka wananchi kumpigia kura ya ndio na kupuuza minong’ono isiyo na mantiki.

Dk. Magufuli anaendelea na ziara yake ya Kampeni katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na ameanza na mikoa ya Kusini.

 

 

Balotelli Atoa Ahadi Ya Kupiga Kazi
Ni Arsenal Vs Spurs Capital One Cup