Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuharakisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya Chamwino mkoani Dodoma na kutaka wataalamu wa TBA watakaochelewesha ujenzi huo kuwekwa mahabusu.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.4 huku akikosoa ushauri uliotolewa na wakala wa majengo nchini (TBA).
“Maendeleo ya kazi ya ujenzi hayaridhishi wakati hela zimetoka siku nyingi na awali zilitolewa dola 1000 za Marekani sawa na shilingi bilioni 2.4 na hazina kukiwa na salio la shilingi milioni 995 kwanini kazi haiendi,” amehoji Rais Magufuli.
Amesema awali ujenzi huo ulitolewa kwa wakala wa majengo nchini lakini makisio yao ya kiasi cha pesa yalikuwa makubwa kwa kudai ujenzi huo ungegharimu shilingi bilioni sita kuliko makisio ya Serikali.
“Kwanini eneo moja lihitaji shilingi bilioni sita? Wakati Hospitali za wilaya tunaweka shilingi bilioni 1.5 na vituo vya afya tunatumia shilingi milioni mia tano na panakuwa na majengo matano hadi sita hii haijakaa sawa,” amefafanua Rais Magufuli.
Kufuatia maelezo hayo Brigedia Jenerali Charles Mbuge ambaye anasimamia ujenzi wa Hospitali hiyo amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati ambapo Rais Magufuli akamkata kuwasweka rumande wataalam wa TBA watakaochelewesha ujenzi.
Akiwa jijini hapa, Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko kuu la Dodoma na kupendekeza soko hilo liitwe soko kuu la Ndugai ambaye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Najua wapo watakao chukia na kutafsiri tofauti lakini mimi dhamiri yangu itafurahi kuona soko hili likiitwa jina la Ndugai maana hata upitishaji wa sheria tumekuwa tukishirikiana nae vizuri,” amebainisha Rais Magufuli.
Ujenzi huo wa soko hilo la kimataifa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 14.4 ambapo mkandarasi amemuhakikishia Rais kuwa kuwa watakamilisha ujenzi kabla ya Februari 15, 2020.