Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, jana aliingia katika jimbo la Hai ambalo linawakilishwa bungeni na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ambapo alifanya mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya watu.

Dk. Magufuli hakusita kumshambulia Mbowe akiwataka wananchi wa jimbo hilo kufanya mabadiliko kwa kumuondoa katika kiti cha ubunge kwa kuwa yeye ni mtalii na mzururaji asiyekaa jimboni humo hivyo hafahamu na ameshindwa kuyatatua matatizo ya wananchi wa jimbo hilo.

Alieleza kuwa mwenyekiti huyo wa Chadema anamkubali yeye na siku zote amekuwa akimsifia hadharani kwa utendaji wake lakini hatakubali kuleta urafiki katika masuala ya maendeleo.

“Mbowe ananipenda na huwa ananisifia hadharani kwamba mimi ni mchapakazi na mimi pia nampenda sana lakini kwenye masuala ya maendeleo ya watanzania sitaweka urafiki, achaneni naye. Mchagueni Dustan Mallya wa CCM awafanyie kazi watu wa Hai,” alisema.

Dk. Magufuli ambaye alipokelewa na mabango yanayoonesha kero za wananchi wa Hai ikiwa ni pamoja na matatizo ya maji na huduma za afya, alisema kuwa kwa kuwa Mbowe amekuwa akizurura Dar es Salaam na Marekani kwa shughuli za chama, ni vyema akapumzishwa ili aendelee kufanya shughuli za kukiimarisha chama chake na nafasi ya ubunge apewe mgombea wa CCM.

Chile Hatarini Kuwakosa Vidal, Sanchez
Liverpool Inasadiki Kwa Jurgen Klopp