Katika kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, Rais dkt. John Magufuli ametangaza kusitishwa kwa mbio za mwenge hadi pale tatizo hilo litakapo kwisha kwani zinakusanya watu wengi sana.
Amesema , Mbio za mwenge zilikuwa zianzie Zanznibar ila hazitaanza na fedha zilizokuwa zitumike katika mbio hizo zitapelekwa wizara ya Afya ili kusaidia katika maandalizi ya kupambana na Corona.
Magufuli amebainisha hayo leo Machi 16, 2020 alipofanya ziara ya kustukiza eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam na maendeleo ya ujenzi wa barabara za juu (Ubungo Interchange).
Amesema “Inawezekana hata akatayeshika Mwenge huo akawa na corona na badala ya Mwenge kuwa wa amani na matumaini ukageuka kuwa Mwenge wa kuhatarisha maisha ya Watanzania.”
Aidha, amesema kama masuala haya ya corona yataisha kabisa basi Mbio za Mwenge zinaweza kufanyika kwa siku hata tatu ila kwa sasa tahadhari ni lazima.
Ktika suala la ujenzi wa barabara za juu (Ubungo Interchange), Rais Magufuli ameelezwa kuwa ujenzi umefikia asilimia 70, huku ukitarajiwa kukamilika kwa gharama ya shilingi Bilioni 230.