Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli amemtengua na baadaye kumsamehe mkuu wa polisi wilaya ya Njombe kutokana na mauaji ya watoto yaliyotokea miezi miwili iliyopita mkoani Njombe na kusababisha doa kubwa nchini na nje ya Tanzania.
Rais Magufuli ametoa uamuzi huo mkoani Njombe wakati akizungumza na wananchi mkoani humo katika uwanja wa sabasaba mjini Njombe.
“hata hili swala la mauaji lilitokea hapa halikutakiwa lichukue mda mrefu hivyo,ndio maana RPC wa hapa nimemtoa wala msitafute sababu nyingine nimemtoa kwasababu alishindwa kusimamia hii kazi,ninataka mambo yawe yanatendeka haraka wewe mtu anapotea mtoto wa kwanza anapotea wa pili mpaka wanafika saba haiwezekani na OCD wa hapa bado yupo naye aondoke najua yuko hapa ananilinda naye sio OCD hapa ni lazima watu wawajibike kila maeneo yao watoto saba wanapote mpaka tunaleta polisi wakina Sabas mkoa wa njombe umepata doa kubwa”alisema Magufuli
Aidha Rais Magufuli amesema kuwa endapo yatatokea mauaji hayo kwa mara nyingine mkuu wa mkoa pamoja na viongozi wengine watawajibishwa.
“Siku nyingine yakitokea ya namna hiyo Mkuu wa mkoa unaondoka,Dc unaondoka,DAS unaondoka katibu tarafa unaondoka mpaka mwenyekiti wa kijiji ikiwezekana na katibu wa CCM wote wanaondoka ili kusudi tufike mahali wote tunachukua hatua mapema,wakina mama waliopotelewa na watoto wao wameumia lakini nitoe wito kwa ndugu zangu huwezi kutajirika kwa kutoa mtoto”aliongeza Magufuli
Hata hivyo Rais Magufuli aliomba mchungaji yeyote kuongoza Toba kwa mkutano huo huku naye akishiriki toba na kuamua kumsamehe OCD huyo.
“Asante sana mchungaji kwa toba na huyo OCD nimemsamehe kutokana na maombi haya abaki hapa hapa naomba RPC umwambie nimemsamehe kutokana na maombi haya naomba asitoke mtu mwingine kufanya mabaya na kila mwananjombe akafanya kazi”alisema Rais Magufuli
Awali mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka aliomba radhi kwa niaba ya wananchi huku akimueleza Rais wale wote waliohusika na mauaji ya watoto wamekwishafikishwa mahakamani
“mheshimiwa Rais ulinipa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama tumeshirikiana nao na hivyo mimi kwa niaba ya wananchi wote wa mkoa wa Njombe nakuomba radhi kutokana na vifo vya watoto saba bila sababu ya msingi lakini tumesimamia kwa nguvu na wote waliohusika kwa sasa wapo mahakamani”alisema Olesendeka
Katika hatua nyingine Magufuli amemkabidhi mkuu wa mkoa wa Njombe rambi rambi kiasi cha shilingi milioni 5 kwa ajili ya familia zilizokumbwa na matatizo hayo.