Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kufuatia vifo vya watu 12, vilivyotokea wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, katika ajali iliyotokea jana majira ya 2:00 usiku baada ya basi kampuni ya City Boy kugongana na Lori aina ya Fuso.
”Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 12 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea jana usiku wilayani Igunga Mkoani Tabora, nawapa pole wafiwa, ndugu jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu mkubwa” amesema Magufuli.
-
Heche aswekwa mahabusu
-
Ndugai ajibu hoja ya kuundwa kwa tume ya kuchunguza matukio ya uhalifu nchini
Pamoja na kutoa pole, amelitaka Jeshi la Polisi, kamati za ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na Mamlaka zote zinazohusika na usalama wa barabarani kujitathmini na kutafuta majibu ya kwa nini ajali za barabarani zinaendelea kutokea kwa uzembe wa uvunjaji wa sheria.
Aidha Rais amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kufikisha salamu zake za pole kwa wafiwa wote na amewaomba Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na majeruhi wote 46 wapone haraka ili waungane na familia zao katika ujenzi wa Taifa.