Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo Jumapili, Februari 2, 2020 ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliopoteza maisha wakati wa kongamano la kidini huko Moshi mkoani Kilimanjaro.
Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya vifo vya watanzania waliopoteza maisha huku akiwaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kurejea katika majukumu yao.
Pia ametuma salamu za pole kwa familia zilizopoteza ndugu katika mafuriko yaliyotokea mkoani Lindi, na kuwataka wakuu wa mikoa yote ambayo imekumbwa na madhara ya mafuriko kufikisha salamu zake za pole kwa familia, ndugu , jamaa na marafiki wote walioguswa na vifo hivyo.
Aidha ametoa wito kwa watanzania wote kuchukua tahadhali katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanasimamia ipasavyo usalama wa raia.