Wakati kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu zikishuhudiwa kuwa na ahadi nyingi na tamu kutoka kwa wagombea urais, ubunge na udiwani kupitia vyama mbalimbali vya siasa, Mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli aliamua kuwapa ukweli wananchi wa mkoa wa Singida.

Akiuhutubia umati wa wananchi waliohudhria mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Mnadani, Ikungi mkoani humo, licha ya kuwaahidi neema ya kukuza uchumi kwa kuunganisha mkoa huo na mikoa yote nchini kwa njia ya barabara, Dk. Magufuli aliwaambia wananchi hao kuwa dawa ya kuondokana na umasikini walionao ni kufanya kazi.

“Siwezi kuwadanganya kwamba ntakuwa nawapa hela mfukoni. Hata Maandiko yanasema ‘asiyefanya kazi na asile’. Na mimi lazima niwaambie ukweli. Kwa kweli tuvitumie hivi vitu vilivyopo katika kujitafutia utajiri. Tukilima mazao yataliwa mpaka Dar es Salaam, mpaka Zanzibar, kwa sababu barabara zipo,” alisema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli aliongeza kuwa katika kuwainua kiuchumi wananchi walio katika mataba ya chini, serikali yake itahakikisha inafuta ushuru na tozo zisizo za lazima kwa wafanyabiashara wadogowadogo pamoja na wakulima.

Alisema serikali yake itahakikisha inafufua na kujenga viwanda nchini ili bidhaa zinazozalishwa nchini ziweze kutengenezwa na kuuzwa kama bidhaa kamili hata nje ya nchi badala ya kusafirishwa kama bidhaa ghafi, ilivyo hivi sasa.

Magufuli ambaye kauli mbiu yake ni ‘Hap Kazi Tu’, ameendelea kuwahakikishia wananchi kuwa endapo ataingia madarakani, watendaji wa serikali yake watakuwa wachapa kazi na asiyeweza kazi ataondolewa mara moja.

Fainali Ya CCM Na Chadema, Majiji Haya Yanahusika
Chadema Yapanga Kulishitaki Jeshi La Polisi