Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwashughulikia wafanyabiashara wote wanaohujumu uchumi wa nchi kwa kutoa risiti za uongo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo akiwa Mkoani Mwanza ambapo mbali na suala la risiti feki, pia ameeleza kuchukizwa na kitendo cha wananchi kununua bidhaa bila kupewa risiti.
“Wananchi mnatakiwa kulipa kodi ili hii miradi ifanyike, kumekuwa na tabia muuzaji anauza bidhaa ya milioni 2 anatoa risiti ya elfu mbili” amesema Magufuli.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la Kigongo-Busisi wa kampuni ya China Civil Engineering Group Limited kujenga usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo ndani ya miaka mitatu badala ya miaka minne ya makubaliano.
Daraja hilo la Magufuli lenye urefu wa Kilomita 3.2 na barabara unganishi ya kilomita 1.66 ni la kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya kukuza uchumi wa nchi.