Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dk John Magufuli ametoa onyo kwa wakimbizi wanaoingia nchini kutoka nchi za jirani na kuingiza silaha kwa lengo la kufanya uhalifu nchini akieleza kuwa atawashughulia ipasavyo atakapoingia madarakani.

Dk. Magufuli alitoa onyo hilo jana wakati akiwahutubia wananchi Mkoani Kigoma katika maeneo ya pembeni mwa mkoa huo yanayowapokea wakimbizi kutoka nchi jirani za Tanzania.

Alisema anatambua kuwa kati ya wakimbizi wanaopata hifadhi nchini, wapo wachache ambao huwa na nia mbaya na kushirikiana na baadhi ya wananchi wa Tanzania wenye nia mbaya kwa lengo la kufanya uhalifu kwa kutumia silaha walizoingia nazo nchini.

“Wale wachache, wenye nia mbaya, wanaoshirikiana na watanzania wachache wenye nia mbaya, serikali yangu itawashughulikia,” alisema na kuongeza kuwa atahakikisha wakimbizi na wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanaishi kwa amani muda wote.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwaahidi wananchi wa eneo hilo kuwa atahakikisha anakamilisha barabara zote kwa kiwango cha lami ili kuondoa usumbufu kwa wananchi ambao wamekuwa wakitekwa na majambazi wakiwa njiani kutokana na urefu wa safari unaowalazimisha kusafiri hadi majira ya usiku kutokana na ubovu wa barabara.

Kutokana na matukio ya utekaji wa mabasi katika mkoa huo, jeshi la polisi limelazimika kusindikiza mabasi yanayosafiri umbali mrefu. Hivyo, Dk. Magufuli aliahidi kurejesha usalama katika safari za mikoa hiyo.

Lowassa Aongeza Idadi Ya Kura, Aendeleza Kilio Cha Wizi Wa Kura
Ukawa Wamjibu Magufuli Kutumia ‘M4C’, Wadai ‘Anatapatapa’