Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa endapo achaguliwa kuwa rais wa Tanzania, atahakikisha anawanyang’anya wawekezaji mashamba wasiyoyaendeleza na kuwagawia wananchi.

Akiwahutubia maelfu ya wananchi mjini Morogoro katika mkutano wa kampeni, Dk Magufuli ameeleza kuwa hatavumilia kuona mashamba pori yaliyochukuliwa na wawekezaji hayaendelezwi wakati wananchi wanahangaika kutafuta ardhi.

Dk. Magufuli alieleza kuwa atafanya zoezi hilo kwa mujibu wa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiwataka wawekezaji kuhakikisha wanayaendeleza mashamba hayo.

“Kama wanaweza waanze kuyalima, walime usiku na mchana ili baada ya tarehe 25 yawe yameshalimwa,” alisema.

Mgombea huyo aliwaomba wananchi kumpigia kura za ndio ili kumuwezesha kuwa rais wa Tanzania kwa kuwa atahakikisha anatatua tatizo la migogoro ya ardhi na kuhakikisha wananchi wanafaidika na ardhi iliyopo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM taifa, Dk Jakaya Kikwete ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikwete: Mnahitaji Rais Mkali
Mzee Makamba Aeleza Lowassa Alivyotaka Kuikacha CCM Mwaka 1995