Rais John Magufuli ameeleza kuwa atafanya kazi kubwa ya kuwabana wezi na mafisadi bila kuwaonea haya ili awe dawa ya tatizo hilo sugu nchini.

Dkt Magufuli ameliita tatizo la rushwa kwa mfano wa ‘jipu’ ambalo ili lipone ni lazima litumbuliwe na kwamba yeye ndiye anayetaka kuwa mtumbua jipu hilo.

“Wananchi wamechukia sana rushwa. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu,” alisema.

“Nawaomba waheshimiwa spika na wananchi mniombee nisione haya wakati ninapokuwa natumbua jipu hilo,” aliongeza.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia Ufisadi.

Alisema kuwa anatambuwa kuwa wananchi wanauchukia sana ufisadi kama anavyouchukia pia na kwamba anaomba washirikiane kwa pamoja kuhakikisha anawabana mafisadi na kuondoa mianya yote ya wizi na ubadhilifu wa fedha za umma.

Katika hatua nyingine, Magufuli ameahidi kupambana na biashara ya dawa za kulevya bila kuwaonea haya wafanyabiashara hao. Alisema kuwa atahakikisha anapambana na wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo badala ya kupambana na watu wadogo.

 

Forbes: Mo Dewji aongoza Kwa Utajiri Tanzania, Dangote Aendelea Kuishika Afrika, Orodha Kamili
Magufuli Awaita Ukawa ‘Watoto’, Spika Awapa Onyo Kali, Asema Atakuwa ‘Mbabe’