Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema serikali haijazuia watu kuvaa barakoa ambapo amewatahadharisha watanzania kutumia barakoa zinazotengenezwa na wizara ya afya au kutumia zilizotengenezwa kwa kitambaa.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Februari 21 jijini Dar es Salaam wakati wa ibada ya dominika ya kwanza ya Kwarezma iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro na kuongozwa na Padre Alister Makubi.

Amesisitiza kwamba barakoa nyingine siyo nzuri, hivyo, waepuke zile wanazoletewa kwa sababu zitawaletea matatizo. Amesema vita ya uchumi ni mbaya, hivyo, wachukue tahadhari wanazoelekezwa.

“Sijasema msivae barakoa wala msini-quote (msininukuu) vibaya, lakini kuna barakoa nyingine siyo nzuri. Nataka niwaambie, huu ndiyo ukweli. Utaletewa barakoa nyingine ambazo zitawaletea matatizo.”

“Ukitaka kuvaa barakoa, vaa zilizotengenezwa na Wizara ya Afya, MSD (Bohari ya Dawa) wanatengeneza barakoa, ukishindwa tengeneza hata ya kwako,” amesema Rais Magufuli.

“Ndugu zangu Watanzania, tujue Mungu yupo, Mungu anaweza kila kitu. Tusiogope, siku moja tutakufa. Hata mimi nitakufa, naweza nikafa kwa corona, naweza nikafa hata kwa magonjwa mengine Ndiyo maana mnaniona sijavaa barakoa, siyo kwamba siogopi kufa,” amesema.

“Msifikiri tunapendwa mno, vita ya uchumi ni mbaya…Tuchukue tahadhari za kiafya kama ambavyo zinatangazwa, tumtangulize Mungu lakini pia tutafute mbadala ikiwa ni pamoja na kujifukizia,” amesema Rais Magufuli.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 22, 2021
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 21, 2021