Mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amewataka watanzania kubeza sera za wagombea wa upinzani wanaodai kuwa serikali ya chama hicho haijafanya kitu katika kipindi chote walichokuwa madarakani.

Akiongea katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi katika jimbo la Chato ambapo ndipo nyumbani kwao, Dk Magufuli alieleza kuwa CCM imeleta mabadiliko makubwa tangu Tanzania ilipopata uhuru ikiwa ni pamoja na ubora wa elimu na miundombinu.

Alisema kuwa wapo wagombea ambao wamekuwa wakibeza kazi iliyofanywa na serikali ya CCM wakati wao walikuwa mawaziri lakini hawakuweza kujenga barabara ya lami jimboni kwao. Alisema kuwa baada ya watu hao kumaliza muda wao, serikali ya CCM ilijenga barabara katika maeneo yao lakini wamesahau na kukosa shukurani wawapo majukwaani.

Chatto 3

Aliwafananisha watu hao wasio na shukurani kwa serikali ya CCM na tabia ya punda, “shukurani ya punda ni mateke.”

Katika hatua nyingine, Dk Magufuli aliiwaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha anamaliza kabisa tatizo la maji kwa kuwa kandarasi anaefanya kazi ya kueleta maji jimboni humo ameendelea kufanya kazi hiyo kwa kasi isiyoridhisha.

Pia, aliahidi kuwa serikali atakayoiunda itahakikisha inainua uchumi wa watanzania wa kima cha chini kwa kuwekeza katika viwanda ili bidhaa ghafi zinazozalishwa na wafugaji kama ngozi na kwato ziweze kutumika katika viwanda vya Tanzania na bidhaa zitakazozalishwa ziuzwe nchi ya nje tofauti na ilivyo sasa ambapo bidhaa ghafi ndizo huuzwa nje ya nchi.

Alieleza kuwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo waliopewa walishindwa kuviendeleza, serikali yake itawanyang’anya na kuwa mali ya serikali ili viendelee kutumika na kutoa ajira kwa wananchi.

Kadhalika, aliwasihi wananchi kuhakikisha wanalinda amani na utulivu uliopo nchini na kutoshawishiwa na wanasiasa kujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kwa Nini Mrembo Wako Anaweza ‘Kukusaliti’ Ingawa Anaonesha Ana Msimamo?
Ahadi Ya Lowassa Yafunika Kigamboni