Serikali nchini, imesema itaendelea na juhudi za kupambana na magugu maji katika Ziwa Victoria ili kudhibiti uhabirifu wa mazingira na athari zitokanazo na uharibifu huo nchini.
Hayo yameelezwa bungeni leo Juni 15, 2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kabula Enock Shitobela aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuondoa magugu yanayosababisha uchafuzi
katika Ziwa Victoria.
Khamis amesema ili kudhibiti magugu maji yasiendelee kuleta athari katika ziwa hilo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Ametaja hatua hizo kuwa ni kutekeleza Mradi wa Hifadhi ya Mazingira katika Ziwa Viktoria (Lake Victoria Environmental Management Project – LVEMP) ambao pamoja na mambo mengine ulitekeleza shughuli zilizolenga kudhibiti magugu maji kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kibaiolojia.
Pamoja na hatua hiyo amebainisha kuwa Serikali inatoa elimu na kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi karibu na ziwa kuhusu namna ya kujitolea katika kazi za kutokomeza magugu maji kila yanapojitokeza ziwani.