Mahabusu wa gereza la Serikali la Hindi, Kaunti ya Lamu wamemuomba Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Mpeketoni, Pascal Nabwana kuwanunulia mbuzi kudhihirisha kile walichodai kuwa ni kusherehekea na kuridhika na utendaji wake wa kazi.
Ujumbe huo ulitolewa na Mahabusu hao baada ya kupata fursa ya kuelimishwa kuhusiana na jinsi ya kupambana na kuzuia itikadi kali na ugaidi magerezani, na jinsi wanavyopaswa kuwa raia wema punde wanapokamilisha vifungo vyao na kurudi mitaani.
Aidha, Mahabusu hao pia walipata fursa ya kuelezea changamoto wanazopambana nazo wakiwa ndani ya jela au kwenye harakati za kuitikia mashtaka yao mahakamani, ambapo Nabwana alionya mahabusu dhidi ya kuendeleza utundu wakiwa gerezani, akishikilia kuwa tabia zao huenda zikaathiri kesi zao.
Ombi la Mbuzi lilitolewa mbele ya maafisa wa idara mbalimbali wakiwemo wa kushughulikia vifungo vya nje, Mahakama, ofisi ya mashtaka ya umma, idara ya usalama, maafisa wa mashirika ya kijamii – Kiunga na maafisa wa kamati za kisheria za kijamii waliozuru gereza hilo ambapo jumla ya Shilingi 5,000 zilichangwa na kukabidhiwa msimamizi wa gereza hilo kwa ajili ya ununuzi wa mbuzi na bidhaa nyingine za wafungwa kufurahia ziara ya maafisa hao.