Washtakiwa watano wa mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na Arusha, Erasto Msuya wamehukumiwa kifo baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya kukusudia kesi ambayo imechukua takribani miaka mitatu.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22 ambako pia lilikutwa gari lake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake mbili.
Katika hukumu iliyosomwa na Jaji Salma Maghimbi Mahakama Kuu iliwahukumu adhabu ya kifo washtakiwa watano na kumuachia huru mmoja.
Jaji Maghimbi alimuachia huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne, maarufu kwa jina la Mredii kutokana na kukosekana ushahidi dhidi yake.
Jaji Maghimbi amesema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo la washtakiwa wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono.
Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa na kusomwa mahakamani yalihusu mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Ally Majeshi.
Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, maelezo ya Sharifu ambayo yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, yanaeleza mpango mzima wa mauaji ulivyosukwa na bunduki ya SMG ilivyonunuliwa.
Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo alieleza namna laini mpya za simu zilivyosajiliwa kwa majina ya Kimasai na namna pikipiki zilizotumika katika mauaji hayo, zilivyonunuliwa.
Kuhusu mshtakiwa wa tatu, Jaji Maghimbi alisema ingawa katika maelezo yake ya kukiri kosa alianza kwa kujitoa na kuwabebesha mzigo washtakiwa wenzake, alishiriki katika nia hiyo ovu.
“Alijua mpango huo wa mauaji na akaendelea kushiriki katika mipango hiyo ya mauaji hadi mwisho bila kujitoa,” amesema Jaji.
“Kitendo cha kutojitoa katika mpango mzima wa mauaji kinaonyesha nia yake ovu ya kutenda kosa hilo. Hakufanya juhudi zozote za kujitoa katika mipango hiyo miovu ya mauaji,” alisema Jaji.
Aidha, Jaji Maghimbi ameendelea kueleza kuwa maelezo ya Karim aliyeeleza kuwa ndiye aliyemfyatulia risasi nyingi Msuya, yanaunganika na yake waliyoeleza Sharifu, Mussa na Majeshi.
Jaji Maghimbi alisema maelezo hayo ya kukiri kosa na maungamo ya washtakiwa, yaliungwa mkono na mashahidi wengine wa Jamhuri na hivyo kuthibitisha shtaka la mauaji pasipo kuacha shaka yoyote.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulioongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavulla uliita mashahidi 27 waliotoa ushahidi kwa kuongea na watano ambao maelezo yao yalisomwa.
Chavulla ambaye alisaidiana na wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana na mawakili Ignas Mwinuka, Kassim Nassir na Lucy Kyusa pia waliwasilisha vidhibiti 26 vya kesi hiyo.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu, wakili wa utetezi Majura Magafu aliiomba mahakama izingatie umri mdogo walionao washtakiwa na kwamba wamekaa muda mrefu gerezani na wanajutia kosa hilo.
Bilionea Msuya aliuawa Agosti 7,2013 kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili eneo la Mjohoroni wilayani Hai.