Ni dhahiri kuwa wanamuziki maswahiba, Ambwene ‘AY’ Yesaya na Hamisi ‘FA’ Mwinjuma watakuwa mabilionea wapya hivi punde, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali rufaa iliyowasilishwa na Kampuni ya simu za mkononi ya MIC (Tigo) ikipinga kuwalipa wasanii hao kiasi cha shilingi 2,185,000,000.

Tigo waliwasilisha rufani yao Mahakama Kuu mwaka jana ikipinga uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala kuitaka kuwalipa wasanii hao kiasi hicho cha fedha kutokana na kutumia nyimbo zao mbili kama miito ya simu kwa nyakati tofauti bila ruhusa yao.

 

Akizungumzia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, mwanasheria wa wasanii hao, Albert Msando aliyekuwa akiwatetea katika kesi hiyo, ameutaja uamuzi huo kama ushindi kwa sanaa ya Tanzania.

“Ni haki yao kulipwa kwa sababu ni kazi zao ambazo zinalindwa kisheria, Msando amenukuliwa.

Mwaka jana, Mahakama ya Wilaya ya Ilala ilitoa uamuzi kuwa Tigo iwalipe wasanii hao kiasi hicho cha fedha na kueleza kuwa uamuzi huo utakuwa fundisho kwa watakaotumia kazi za sanaa (Intellectual property) bila ruhusa ya wamiliki.

Hata hivyo, Tigo hawakurishishwa na uamuzi huo wa mahakama na kuamua kukata rufaa Mahakama Kuu ambayo leo imebariki rasmi uamuzi huo.

Uamuzi huu wa makahama kwa kesi ya kazi za wasanii ni wa kwanza kuwa na kiasi kikubwa cha fedha kama fidia kwa wasanii na utaweka historia katika sekta ya sanaa Afrika Mashariki.

Hukumu hii inaaweza kutumika kutolea maamuzi kesi nyingine zinazofanana na kesi hii (precedent).

Hata hivyo, Tigo wana nafasi ya kukata rufaa tena kwenye Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi huo.

Tanzania yatajwa kuwa eneo bora la vivutio Afrika
Video: Fanyeni kazi usiku na mchana kukamilisha barabara ya Kibondo-Nyakanazi-JPM