Mahakama Kuu nchini Kenya leo imeamuru kufutwa kwa marufuku ya kuzuia daladala maarufu kama matatu, kuingia katikati ya jiji la Nairobi.
Jaji Wilfrida Okwany ametoa uamuzi huo na kueleza kuwa ingawa Serikali imesitisha marufuku hiyo, bado haifahamiki ni lini tena itarejea uamuzi wake wa kuzuia usafiri huo kuingia katikati ya jiji.
Uamuzi huo ni matokeo ya kesi iliyofunguliwa Jumatatu na mfanyabiashara Paul Kobia pamoja na wamiliki 21 wa matatu. Walalamikaji hao walidai kuwa marufuku hiyo ilikuwa na sababu ambazo hazikuwa na mashiko.
Wakazi wa jiji la Nairobi walilazimika kutembea kwa miguu umbali mrefu kidogo kufuatia marufuku hiyo, ambapo vituo vipya vya kushushia abiria vilipangwa katika maeneo tofauti kabla ya kuingia katikati ya jiji hilo. Wakaazi hao walilalamika wakidai kuwa wamepata adhabu ya kutembea umbali mrefu na kuzua hofu ya kuchelewa kazini.
Ingawa awali, Gavana wa Nairobi Mike Sonko aliweka msimamo kuwa kitendo cha wananchi kutembea kingewasaidia pia katika kufanya mazoezi, mapema leo alisimamisha kwa muda marufuku hiyo na kueleza kuwa ameguswa na malalamiko ya wananchi.
“Nimeguswa na malalamiko ya wakaazi wa Nairobi kutokana na zuio la matatu, na ninatangaza kuwa utekelezaji wa agizo la zuio hilo umesitishwa mara moja,” alisema Sonko.
Awali, Serikali ilisema kuwa inazuia matatu, pikipiki na bajaji kuingia katikati ya jiji ili kupunguza msongamano katikati ya jiji hilo.