Taasisi sita ambazo ni Kituo cha Sheria na Haki za binadamu ( LHRC), Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Baraza la Habari la Tanzania (MCT), Jamii Media, Jumuiya ya Waandishi wa Habari WanawakeTanzania (TAMWA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania Editors (TEF) zimewashitaki Waziri wa Habari, Mamlaka ya Udhibiti Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali juu ya Kanuni za maudhui ya kimtandao 2018.
Taasisi hizo zimefikisha malalamiko yake katika Mahakama kuu ya kanda ya Mtwara juu ya matumizi ya maudhui hayo ya mtandaoni ambapo wamiliki wanatakiwa kuwa wamejisajiri ili kupata ridhaa ya kutoa matangazo yao kupitia mtandaoni.
Kufuatia kesi hiyo Mahakama Kuu Mtwara imetoa zuio la muda la matumizi ya kanuni za maudhui ya kimtandao 2018, ambazo matumizi yake yalipaswa kuanza rasmi Mei 5.
Taasisi hizo zimewakilisha mahakamani maombi ya kuzuia matumizi ya Kanuni hizo April 30, mwaka huu na Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa Mei 10, 2018.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania katika maombi ya msingi taasisi hizo zinaiomba Mahakama Kuu kufanya mapitio ya kanuni hizo kwa kigezo kwamba; waziri ametumia nguvu ya kisheria nje ya mamlaka yake ( Ultra vires), Zinakiuka kanuni za usawa (natural justice), Kanuni hizo zinapingana na haki ya kujieleza, haki ya kusikilizwa, na haki ya usiri.