Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya leo imetengua hukumu, Mwenendo na Kifungo alichohukumiwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ kwa kueleza kuwa ni kutokana na ubatili wa mwenendo wa kesi hiyo.
Hukumu yake imesomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Jaji Utamwa amesema kuwa hakubaliani na hoja za upande wa Serikali ambao ndio wajibu rufaa.
Jaji Utamwa amesema, kulikuwa na makosa yasiyotibika katika mwenendo wa shauri hilo, hasa pale aliyekuwa Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya aliposhindwa kuwasomea mashtaka washtakiwa katika hatua za awali.
Aidha, amesema kwamba mapungufu hayo, yaliathiri mwenendo mzima wa kesi iliyopelekea kufungwa kwa Sugu na mwenzake Emmanuel Masonga na hivyo ametengua hukumu yao.
Hata hivyo, Sugu aliyehukumiwa kifungo cha miezi mitano jela katika Kesi hiyo alitumikia miezi minne na kutoka kwa msamaha wa Rais alioutoa mnamo Aprili 26, 2018 katika maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano.
Mwezi Februari mwaka huu, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga walihukumiwa kifungo cha miezi mitano na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.