Majaji nchini Marekani wamemkuta na hatia afisa wa polisi wa zamani Derek Chauvin (45), kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi George Floyd kilichotokea Minneapolis mwaka 2020.

Chauvin alinaswa katika picha za televisheni akiwa amemkandamiza shingoni Floyd kwa kutumia goti kwa zaidi ya dakika tisa.

Video hiyo iliyotazamwa sana iliibua hisia kali na kusababisha maaandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi kote duniani na utumiaji wa nguvu kupita kiasi unaofanywa na kikosi cha polisi.

Chauvin alipatikana na makosa matatu: mauaji ya kiwango cha pili, kiwango cha tatu na mauaji bila kukusudia.

Atasalia kizuizini hadi atakapohukumiwa na huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.

Jopo la majaji 12-lilikaa kwa siku moja kujadili na kufikia uamuzi huo na baada ya pande zote kutoa kauli zao za mwisho, majaji walijitenga katika hoteli kujadili kwa makini uamuzi wao.

Uamuzi huo ulishangiliwa kwa vifijo na nderemo nje ya mahakama, ambako mamia ya watu walikuwa wamejitokeza kufuatilia tangazo hilo.

Wakili wa familia ya Floyd, Ben Crump, amesema ni hatua ya “muhimu katika historia” ya Marekani. ameandika katika mtandao wa twitter. Rais Joe Biden na makamu wake Kamala Harris waliipigia simu familia ya Floyd mara baada ya uamuzi huo.

Biden alisikika akisema “hatimaye haki imetendeka, tutaongeza juhudi kuhakikisha mengine yanafikiwa. Hii itakuwa hatua ya kwanza muhimu ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi uliokithiri katika mifumo yetu,” amesma Biden.

Wakati huo huo, Kamala Harris aliwahimiza wabunge kupitisha muswada wa George Floyd unaolenga kurekebisha idara ya polisi nchini Marekani.

“Muswada huu ni sehemu ya urithi wa George Floyd. Kazi hii ni ya muda mrefu,” alisema Kamala.

Chauvin ambaye ametolewa mahakamani akiwa katiwa pingu anasubiri hukumu yake itakayotolewa wiki 8 zijazo.

FIFA yaipa Simba SC siku 14
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 21, 2021