Mahakama nchini Brazil imemuamuru Rais wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro kumlipa fidia mwandishi wa habari wa kike kwa kumtolea maneno ya kumdhalilisha.

Uamuzi huo wa Mahakama umekuja kufuatia kauli aliyoitoa Rais Bolsonaro dhidi ya Patricia Campos Mello ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Folha de S.Paulo, kuwa alikihonga rushwa ya ngono chanzo chake cha habari ili kimpe taarifa zenye mlengo hasi dhidi yake.

Katika uamuzi huo wa Mahakama, Jaji alisema maneno ya Rais Bolsonaro yalilenga kumvunjia heshima mwandishi huyo wa habari.

Hivyo, iliamua kuwa Rais huyo amlipe $3,500 (sawa na Shilingi 8,116,500 za Tanzania) kama fidia, na kwamba anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama, mwandishi huyo wa habari wa kike, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa ‘uamuzi huo wa mahakama ni ushindi kwa wanawake wote nchini humo’.

Rais Bolsonaro aliingia madarakani Januari 2019, na amekuwa na mvutano na baadhi ya waandishi wa habari hasa kuhusu jinsi wanavyoripoti taarifa zenye mlengo hasi dhidi ya utawala wake.

Kesi ya mwanamke aliyesukumwa kutoka ghorofa ya 12 kwa kukataa ngono yakitafuta kituo cha radio
Rais Samia amsimamisha kazi Mkurugenzi mkuu TPA