Maandalizi ya Mahakama ya Mafisadi iliyoahidiwa na Rais John Magufuli yamefikia katika hatua nzuri na muda wowote inaweza kuanza kwa kutumia muundo wa ndani ya mahakama zilizopo kwa lengo la kuhakikisha inatekeleza majukumu yake bila kuingiliwa.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato huo wa Mahakama ya Mafisadi, muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Jaji Mstaafu Damian Lubuva aliyetembelea wizara yake kwa lengo la kushauri kuhusu muundo wa mahakama hiyo.
Dk. Mwakyembe alieleza kuwa bado wananchi wana imani kubwa na Mahakama zilizopo hivyo mahakama hizo za mafisadi zitaanza kutekeleza majukumu yake kwa kutumia miundo iliyopo.
Kwa upande wake Jaji Mstaafu Lubuva, alisema kuwa Mahakama zinapaswa kuwa chombo kinachoaminika na wananchi katika kutekeleza majukumu yake na kwamba hakitaweza kuamika endapo kitatoa hukumu batili.
Muundo wa mahakama ya Mafisadi na Wahujumu Uchumi ni moja kati ya ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wote wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Tayari ameanza kuifanyia kazi kwa vitendo ikiongezwa nguvu na operesheni ‘tumbua majipu’.